MAAFISA UNUNUZI NA UGAVI TEMESA WAPIGWA MSASA MFUMO WA TIMIS-MUM
Posted On: August 20, 2026
Meneja wa Umeme na Elektroniki kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Mhandisi Pongeza Semakuwa, leo tarehe 20 Agosti, 2026 amewapatia mafunzo Maafisa Ununuzi na Ugavi kuhusu maboresho yanayoendelea kufanyika katika Mfumo wa TEMESA wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo TIMIS-MUM.
Mafunzo hayo yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa TEMESA Makao Makuu jijini Dodoma, yanashirikisha Maafisa Ununuzi kutoka ofisi za mikoa na vituo vyote vya TEMESA nchini.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mhandisi Semakuwa ameeleza kuwa mfumo wa TEMESA TIMIS-MUM unaendelea kufanyiwa maboresho ya mara kwa mara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kuhakikisha wateja wanapata huduma bora kwa urahisi, uhakika na kwa wakati, bila usumbufu.
Miongoni mwa mada zilizofundishwa katika mafunzo hayo ni, Moduli za Ugavi na Ununuzi kwenye mfumo wa TEMESA TIMIS-MUM |(Modules for Supplies and Procurement), Moduli za Maombi ya Mafuta ya Rasilimali Watu (Modules for Human Resource Fuel Requests), Moduli za Mahitaji ya Nyenzo za Mradi ( Modules for Project Material Requisition) pamoja na kuwafundisha badhi ya makosa yanayojitokeza mara kwa mara (Frequently Observed Mistakes) katika matumizi ya mfumo.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika kuimarisha matumizi sahihi na yenye ufanisi ya mifumo ya kidijitali, kuongeza uwajibikaji na kuboresha huduma kwa wateja.