WIZARA YA UJENZI YAUNGA MKONO MAGEUZI TEMESA
Posted On: August 13, 2026
Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi na Umeme wa Wizara ya Ujenzi, Qs. Mwanahamisi Kitogo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mhe. Balozi Aisha Amour, amepongeza uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa hatua zinazochukuliwa kuboresha utendaji na utoaji wa huduma.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kikao kazi cha Uongozi wa TEMESA (Management Retreat) mkoani Morogoro, Qs. Mwanahamisi amesema Wizara imeridhishwa na maboresho yanayoendelea, ikiwemo matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Matengenezo (MUM) unaosaidia kuongeza uwazi, ufanisi na tija.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa taasisi za Serikali kutumia huduma za TEMESA kwa kuzingatia matakwa ya sheria, huku akiahidi ushirikiano wa Wizara katika kuboresha huduma za Vivuko, Miundombinu, Rasilimaliwatu na utekelezaji wa miradi ya PPP na mashirikiano na Sekta binafsi.
“Serikali inawaamini, na mimi nina imani na uongozi wa sasa wa TEMESA. Ninawategemea kuleta mageuzi makubwa ya kiutendaji,” amesema Bi. Mwanahamisi.
Kikao kazi cha Mameneja wa TEMESA nchi nzima kilichofanyika kwa siku tatu Mkoani Morogoro kimehitimishwa rasmi tarehe 12 Agosti 2026.