KATIBU MKUU WIZARA YA UJENZI AIPONGEZA TEMESA KWA MATUMIZI YA MIFUMO, AITAKA KUONGEZA USHIRIKIANO NA SEKTA BINAFSI
Posted On: August 14, 2026
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, ameupongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa hatua ya kutumia mifumo katika utoaji wa huduma, akisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia ni muhimu katika kuongeza ufanisi, uwazi na kasi ya utoaji wa huduma ili kufikia malengo ya kutekeleza Dira 2050 ya maendeleo ya taifa..
Balozi Aisha ameyasema hayo leo, Agosti 14, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa ofisi za TEMESA Makao Makuu jijini Dodoma, ambapo ameitaka TEMESA kuendelea kuboresha na kuimarisha matumizi ya mifumo katika shughuli zake zote, kwa kuwa Serikali inalenga kuongeza matumizi ya teknolojia katika uendeshaji wa taasisi na utoaji wa huduma.
“Nimefurahishwa na matumizi ya mifumo, kwa sababu tumekuwa na mikakati mingi ya kuhakikisha tunafanya kazi kwa kutumia mifumo. Siku hizi si lazima uwe ofisini ili kupata taarifa, kupitia mifumo unaweza kupata taarifa kwa urahisi na kwa wakati. Kwa hiyo, mwelekeo wetu ni kuhakikisha kila kitu kinaendeshwa kwa kutumia mifumo. Serikali inataka tufike huko. Tunapokuwa na mifumo, taarifa zinapatikana kwa uhakika na kwa haraka,” amesisitiza Balozi Aisha.
Aidha, Balozi Aisha ameitaka TEMESA kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi katika utekelezaji wa majukumu yake, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuongeza tija, ubunifu na ufanisi, pamoja na kuipunguzia Serikali mzigo wa utekelezaji wa baadhi ya majukumu.
“Kwa hii kasi tunayoendanayo mashirikiano na Sekta binafsi hayakwepeki. Hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza katika kutekeleza malengo ya Dira 2050 ni lazima kuzingatia ushirikiano na Sekta binafsi ili kukuza huduma zetu”, amesema Balozi Mha. Aisha.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Bw. Kheri Mahimbali, amesema Wakala umejipanga kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na Wizara, wadau na Sekta binafsi ili kutekeleza dira ya maendeleo ya taifa na kuhakikisha inafikia malengo yake katika kutoa huduma bora, zenye ufanisi na zinazokidhi mahitaji ya wananchi.