TEMESA YAINGIA MAKUBALIANO NA AZAM MARINE KUTATUA KERO YA VIVUKO MAGOGONI

News Image

Posted On: June 13, 2022

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umezindua rasmi ushirikiano baina yao na kampuni ya Azam Marine ambao utawawezesha kutumia vivuko vya Azam Marine kwa ajili ya kupunguza kero ya usafiri kwa wananchi wa Kigamboni Jijini Dar es Salaam wakati wakiendelea kufanya ukarabati wa vivuko vingine.

Akizungumza baada ya kufanya makubaliano hayo leo Juni 13,2022 Jijini Dar es Salaam Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro N. Kilahala, amesema wamekabidhiwa vivuko viwili ambavyo kila kimoja kinauwezo wa kubeba watu 250 kwa wakati mmoja hivyo basi kupitia vivuko hivyo wataweza kufanya safari mara nyingi zaidi kwa siku kwakuwa vivuko hivyo vinatembea kwa haraka zaidi.

Amesema kuna gharama ambazo wamekubaliana na Azam ambazo TEMESA watalipa huku watumiaji wa huduma hiyo wakiendelea kulipa gharama zilezile za awali za shilingi mia mbili kwa safari moja.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Azam Marine Bw. Aboubakar Salim amesema wameona kuna umuhimu mkubwa wa kuingia makubaliano na TEMESA kwasababu kumekuwa na changamoto ya vivuko kwa upande wa Magogoni na Kigamboni na hivyo kupitia makubaliano hayo wataweza kupunguza kero hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe.Fatma Nyangasa ameipongeza Azam Marine kwa kukubali ushirikiano huo kwani watasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kero ya vivuko kwenye eneo la Kigamboni.

Aidha amesema Serikali imekuwa ikiendelea kufanyia kazi changamoto moja baada ya nyingine ndo maana wakaamua kuingia makubaliano na Kampuni ya Azam Marine ikiwa ni moja wapo ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

"Serikali tayari imekwisha tenga fedha kwaajili ya kununua kivuko kikubwa zaidi ya MV. MAGOGONI ambayo itakuwa inauwezo wa kubeba abiria wengi zaidi pamoja na vyombo vingi vya usafiri kwa wakati mmoja". Amesema Mhe.Nyangasa.

Vivuko hivyo kutoka Azam, vitafanya kazi kwa pamoja na vivuko vya MV.MAGOGONI pamoja na MV. KIGAMBONI mpaka hapo kivuko cha NV. KAZI kitakaporejea kutoka katika ukarabati mkubwa.