MTENDAJI MKUU TEMESA AFANYA ZIARA KARAKANA ZA TEMESA ARUSHA NA KILIMANJARO
Posted On: October 08, 2026
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Bw. Kheri Mahimbali, amefanya ziara ya kikazi katika ofisi zaTEMESA mkoa wa Arusha na Kilimanjaro akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya TEMESA kutoka Makao Makuu.
Ziara hiyo ya kikazi imelenga kutembelea na kukagua shughuli zinazotekelezwa katika mikoa hiyo, pamoja na kuzungumza na watumishi kwa lengo la kusikiliza changamoto, mapendekezo na maoni mbalimbali kuhusu utekelezaji wa majukumu na utoaji katika huduma.
Katika ziara hiyo, Mtendaji Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa uweledi na ufanisi huku akiahidi kuendelea kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya watumishi. Ameeleza kuwa ustawi wa watumishi ni sehemu muhimu katika kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ubora katika huduma zinazotolewa na TEMESA.
“Ninapenda kutumia nafasi hii kuendelea kukumbushana misingi bora ya utumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa uadilifu, uweledi na ufanisi mkubwa huku kwa upande wa utawala tukiendelea kufanya maboresho ya kimaslahi pamoja na mazingira ya kazi kwa ustawi wa watumishi na kuhakikisha tunakuwa na vifaa bora na vya kisasa kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia”. Amesema Mahimbali
Kwa upande wake, Meneja wa Utawala, Bw. Starnely Mulibo, aliwasihi watumishi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ili kuhakikisha wanaendelea kuleta matokeo chanya hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko na kueleza kuwa utendaji mzuri wa watumishi ni muhimu katika kuimarisha ukuaji wa taasisi.
Ziara hiyo imekuwa fursa muhimu kwa uongozi wa TEMESA kusikia moja kwa moja maoni ya watumishi wa Arusha na Kilimanjaro, kutambua changamoto zinazowakabili pamoja na kuweka msisitizo wa ushirikiano kati ya uongozi na watumishi kwa lengo la kuongeza ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa na Wakala.