​MKUU WA MKOA WA KATAVI AFUNGA MAONESHO YA MWANAKATAVI, AIPONGEZA TEMESA KWA UTOAJI WA HUDUMA BORA

News Image

Posted On: November 01, 2026

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amefunga rasmi Maadhimisho ya Tano ya Wiki ya Mwanakatavi, yaliyoambatana na Maonesho ya shughuli, kazi na bidhaa mbalimbali, huku akiupongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa ubora wa huduma za matengenezo ya magari, mifumo ya umeme na vifaa vya elektroniki zinazotolewa Mkoani humo.

Akizungumza wakati wa alipotembelea banda la TEMESA katika Maonesho hayo, Mhe. Mrindoko amepongeza juhudi na weledi wa Wakala huo katika utoaji wa huduma, akieleza kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa taasisi zinazonufaika na huduma za matengenezo ya magari zinazotolewa na TEMESA.

“Niwapongeze TEMESA kwa kazi nzuri mnayoifanya hapa Mkoani Katavi, mimi binafsi, katika Ofisi yangu ya Mkuu wa Mkoa, hakuna mtu anayefanya kazi nje ya TEMESA, magari yetu tunayafanyia matengenezo TEMESA, nawafahamu na mnafanya kazi nzuri kwa hiyo hongereni sana na muendelee kuboresha huduma zenu,” amesema Mhe. Mrindoko.

Pongezi hizo ni kielelezo cha imani ambayo taasisi za Serikali zinaendelea kuwa nayo kwa TEMESA katika kutoa huduma za kiufundi zenye ubora, ufanisi na zinazokidhi mahitaji ya wateja wake.

Maadhimisho ya Tano ya Wiki ya Mwanakatavi yalianza Oktoba 25, 2026 na kuhitimishwa Oktoba 31, 2026, yakiwa na lengo la kutangaza fursa za utalii, uwekezaji na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika Mkoa wa Katavi.

Maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo: “Katavi Yetu: Talii, Wekeza, Imarisha Uchumi kutekeleza Dira ya Taifa 2050.”