MTENDAJI MKUU TEMESA AWATAKA WATUMISHI KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KWA UFANISI

News Image

Posted On: May 14, 2026

Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Bw. Kheri Mahimbali, amewataka watumishi wa taasisi hiyo kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kutenda mema katika utumishi wa umma, huku akisisitiza kuwa kutenda wema ni msingi wa kujenga mazingira bora ya kazi na kulipwa wema katika maisha na utumishi kwa ujumla.

Akizungumza na watumishi katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 12 Mei, 2026 katika ukumbi wa TEMESA Makao Makuu jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu alisema kuwa nidhamu, kujituma na mahusiano mazuri kazini ni nguzo muhimu za mafanikio ya taasisi pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi na wadau mbalimbali.

“Tutende wema katika kazi zetu, tushirikiane na tuheshimiane, kwani ukitenda wema una nafasi kubwa ya kulipwa wema. Tunapofanya kazi kwa moyo mzuri na kwa uadilifu tunajenga taasisi imara na mazingira bora kwa wote,” alisema Bw. Kheri.


Mtendaji Mkuu aliongeza kwa kusema kuwa kila mtumishi ana wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi huku akizingatia maadili ya kazi, ushirikiano na moyo wa kusaidiana ili kuendelea kuijenga na kuilinda taswira njema ya TEMESA.

Aidha, Mtendaji Mkuu alimshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kumuamini na kumteua kushika nafasi hiyo, akiahidi kufanya kazi kwa bidii, uwazi na ushirikiano ili kuhakikisha taasisi inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.


Kwa upande wao, baadhi ya watumishi walieleza utayari wao wa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii huku wakizingatia maelekezo na miongozo inayotolewa na uongozi wa taasisi hiyo.