​TEMESA YAKUTANISHA WADAU KUJADILI FURSA MATUMIZI YA MAGARI YA NISHATI YA UMEME NCHINI

News Image

Posted On: August 31, 2026

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) leo tarehe Agosti 31, 2026 umeendesha kikao cha wadau cha kujadili fursa za matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme (FIRST E-MOBILITY MULTI-SECTORAL), kikao hicho kilicholenga kujadili maendeleo, fursa na changamoto katika matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme nchini Tanzania kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Makao Makuu TEMESA jijini Dodoma na kuwakutanisha wadau mbalimbali kutoka Serikali na sekta binafsi, wakiwemo watengenezaji, waagizaji na wasambazaji wa magari ya umeme pamoja na bajaji.

Akizungumza kwa Niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ufundi, Mhandisi Julius Humbe amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kujenga mazingira wezeshi kwa maendeleo ya usafiri unaotumia nishati ya umeme nchini ili kupunguza matumizi ya nishati ya petroli na diseli ambazo zimekuwa changamoto kubwa kwa sasa.

‘’Mtakumbuka kwamba kuna tatizo kubwa kuhusu bei za mafuta kupanda hivyo sisi kama wadau tumeona ni muhimu kuwakutanisha wadau ili tuweze kujadili kuhusu matumizi ya vyombo vyinavyotumia nishati ya umeme,kulingana na Dira yetu ya Maendeleo ya 2050, tunasema tunaenda kidigitali zaidi, tunatamani Serikali ipate magari yanayotumia umeme ili tuweze kupunguza gharama za uendeshaji katika Serikali yetu’’, amesema Mhandisi Humbe.

Ameongeza kuwa teknolojia hiyo ya magari yanayotumia nishati ya umeme yanatumia kiasi kidogo sana cha nishati ya umeme na hivyo yatasaidia katika uendeshaji wa magari ya Serikali kwa kuwa kwa nishati kidogo tu ya umeme magari hayo yanao uwezo wa kusafiri kwa zaidi ya kilometa 600 kwa mujibu wa wataalamu walioleta magari hayo kwa ajili ya kuyaonesha.

Mhandisi Humbe ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha teknolojia ya magari ya umeme inaendelezwa kwa kuzingatia mahitaji ya nchi, usalama, viwango na upatikanaji wa miundombinu rafiki kwa watumiaji. Aidha, wadau walijadili masuala mbalimbali yanayohusiana na miundombinu ya kuchajia magari ya umeme, matengenezo na huduma za kitaalamu, viwango na usalama wa magari ya umeme, upatikanaji wa vipuri pamoja na uendelezaji wa wataalamu wenye ujuzi wa teknolojia ya E-Mobility.

Wadau hao waliishukuru TEMESA kwa kuwapatia fursa hiyo ya kuwakutanisha pamoja ili waweze kutangaza bidhaa zao za magari na vyombo vinavyotumia umeme. Kikao hicho kimekuwa fursa kwa Serikali na wadau wa sekta binafsi kubadilishana uzoefu, kutambua changamoto zilizopo na kuweka msingi wa ushirikiano zaidi katika kukuza E-Mobility nchini Tanzania.

Miongoni mwa kampuni zilizoshiriki kikao hicho ni Dow Elef Auto Limited, BYD Tanzania (Harmony Auto Branch), JMC Tanzania (Transinnovation Motors Tanzania), Plug and Ride Company Limited, GAC Tanzania (HF Motors Tanzania), E Motion Africa Limited na Tanzania Jetour.