​KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI NA MITAJI YA UMMA YAFURAHISHWA NA MABORESHO KARAKANA YA TEMESA DODOMA

News Image

Posted On: August 28, 2026

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma leo tarehe 26 Agost 2026, imetembelea Karakana ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kujionea huduma zinazotolewa na TEMESA katika karakana hiyo na maboresho yanayoendelea kufanyika.

Wakati wa ziara hiyo, Kamati imepongeza jitihada za Serikali katika kuiimarisha TEMESA na imeeleza kufurahishwa na maboresho na hali ya huduma waliyoiona katika Karakana ya TEMESA Dodoma.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Masanja Kadogosa (Mb), ameipongeza Serikali kwa hatua zinazochukuliwa kuimarisha TEMESA na kuitaka kuendelea kuzingatia maoni na ushauri wa Wabunge ili kuongeza ufanisi wa huduma.

‘’Mimi binafsi naifahamu TEMESA ilipokuwa miaka ya zamani, kwa sasa naona mabadiliko makubwa, nashauri mjikite zaidi kwenye kutoa mafunzo kwa mafundi wenu ili waweze kwenda na teknolojia ya magari ya kisasa’’ amesema Kadogosa.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amewashauri Wabunge kutumia huduma za TEMESA kwa kuleta magari yao kwa ajili ya matengenezo ili waweze kujionea kwa vitendo ubora wa huduma.

“Nishauri ndugu zangu wabunge nyinyi ndio watu wa kwanza kujua kama huduma zimeboreshwa, leteni magari yenu TEMESA mtaona haya mabadiliko kwa nadharia,’’ Amesema Dkt. Msonde

Ziara hiyo iliyohudhuriwa pia na baadhi ya wajumbe wa menejimenti ya TEMESA ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati ya kufuatilia utendaji wa taasisi za Umma na kutoa ushauri unaolenga kuimarisha ufanisi na mchango wa taasisi hizo katika maendeleo ya Taifa.