MWENYEKITI WA BODI AITAKA MENEJIMENTI YA TEMESA KUIMARISHA UADILIFU NA KUCHOCHEA MABORESHO YA TAASISI

News Image

Posted On: October 23, 2026

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Bw. Andrew Massawe, amewataka wajumbe wa Bodi na Menejimenti kushirikiana kwa dhati katika kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo ili kuongeza ufanisi na kuendelea kutoa huduma bora kwa Serikali na wananchi.

Akizungumza katika kikao cha Bodi kilichofanyika Oktoba 22, 2026, katika ofisi za TEMESA Makao Makuu jijini Dodoma, Bw. Massawe amesisitiza umuhimu wa Menejimenti kuimarisha mabadiliko ya kiutamaduni na kitabia (cultural transformation) kwa kujenga misingi imara ya uaminifu, uadilifu na uwajibikaji. Amesema mabadiliko hayo ni muhimu katika kuchochea maboresho ya taasisi na kufanikisha malengo yaliyowekwa.

“Menejimenti inapaswa kuimarisha utendaji kazi wake kwa uaminifu, uadilifu na uwajibikaji , huku ikijiepusha na vitendo vinavyoweza kuhujumu taasisi, hatuwezi kubali wachache waendelee kuichafua taasisii, kuharibu taswira yake na kudhoofisha imani ya wananchi kwa TEMESA. Kila mmoja wenu ana wajibu wa kulinda heshima na maslahi ya taasisi kwa kuzingatia maadili na weledi katika utekelezaji wa majukumu na kwa maslahi mapana yaTaifa,” amesisitiza Bw. Massawe.

Aidha, Mwenyekiti ameipongeza Menejimenti kwa matokeo chanya yaliyopatikana kupitia kikao kazi cha Mameneja na mameneja wa Mikoa kilichofanyika mkoani Morogoro. Amehimiza kuendelezwa kwa vikao kazi hivyo ili kuimarisha uwezo wa mameneja, kuhamasisha kubadilishanauzoefu na kuongeza ufanisi katika usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya taasisi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Bw. Kheri Mahimbali, ameishukuru na kuipongeza Bodi ya Ushauri kwa mchango wake katika kuishauri Menejimenti na kuwezesha kupatikana kwa matokeo chanya katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi ambapo amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo ili kufanikia malengo ya TEMESA katika kutoa huduma bora kwa Serikali na wananchi.