WASIMAMIZI WA VIVUKO TEMESA WAPATIWA ELIMU YA HALI YA HEWA KUIKABILI EL NINO
Posted On: October 21, 2026
Wakuu wa vivuko, waendesha vivuko na wasimamizi wa vivuko kutoka vituo vyote vya TEMESA hapa nchini, tarehe 20 Septemba, 2026 wamepatiwa elimu kuhusu masuala ya hali ya hewa pamoja na usalama wa vyombo vya usafiri majini. Mafunzo hayo na elimu yametolewa na wataalamu wa hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) pamoja na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na yamefanyika katika ofisi za Makao Makuu ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) mjini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Bw. Kheri A. Mahimbali, amesema kuwa Serikali imetoa maelekezo mbalimbali kuhusu ujio wa mvua za El'nino hivyo TEMESA imeona umuhimu wa kipekee wa kuwaita kwa pamoja wataalamu hao ili waweze kutoa elimu pamoja na tahadhari za kiusalama kwa wakuu hao wa vivuko pamoja na waendesha vivuko.
‘’Serikali imetoa maelekezo mbalimbali kuhusiana na ujio wa mvua hizi za El’nino, kwasababu hiyo TEMESA tumeona ni vyema tukutane kwasababu sisi ni moja ya sehemu muhimu na za mwanzo ambazo zitaweza kuathirika zitakapokuja mvua hizo kali, tumeona badala ya sisi kuanza kutoa matamko basi kwanza tuongee wenyewe kwasababu nyie ndio wadau wetu, tumewaalika nyie watalamu kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) pamoja na wataalamu kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwasababu ni wadau muhimu katika hilo eneo, TASAC kama msimamizi wetu lakini pia kama mlezi wetu kwenye hii sekta ya usafiri Majini, na TMA ndio mdau muhimu kwasababu yeye ndiye anaetuhabarisha kuhusu matarajio ya Hali ya hewa.’’ Amesema Mtendaji Mkuu.
Naye Meneja wa Kanda ya Kati kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Bw. Mussa Kidato amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa kwa upande wa wataalamu na usimamizi wa mambo ya hali ya hewa jambo linaloifanya Mamlaka hiyo kuwa miongoni mwa Mamlaka bora katika Ukanda wa Afrika na mpaka sasa Mamlaka hiyo inazo rada mpya tano za kisasa ambazo zinaisaidia kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa ufanisi mkubwa huku nyingine zikiwa tayari zimeagizwa na zinatarajiwa kufika Nchini wakati wowote kuanzia sasa.
Bwana Kidato ameongeza kuwa hali ya ongezeko la joto katika bahari inayotokea katika maeneo ya kitropiki ndio ambayo inasababisha uwepo wa mvua kubwa katika ukanda wa Afrika ya Mashariki hivyo ni muhimu sana wakuu hao wa vivuko kupatiwa elimu hiyo ili kuweza kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na uwepo wa mvua hizo kubwa.
‘’Yapo maeneo ambayo tayari yameanza kupata hizo mvua kubwa, yametokea mafuriko makubwa na baadhi ya watu wameweza kupoteza maisha kwahiyo ni muhimu sisi kujiandaa ili kukabiliana na hali hiyo endapo itatokea katika Ukanda wetu.’’ Amesema Bw. Kidato.
Aidha Bwana Kidato ameongeza kuwa Suala la El’nino, Mamlaka hiyo ilianza kuwa na taarifa nalo mapema kupitia mifumo yao na wataalamu wao tayari walichakata na kuona uwepo wa El’nino kuanzia mwezi Aprili mwaka huu, tayari walianza kuchukua hatua muhimu kwa sekta mahsusi ili kuweza kuzifahamisha kuhusu nini kinachokuja ikiwemo Serikali kwa ajili ya kujiandaa na mvua hizo kubwa.
Elimu hiyo na mafunzo imelenga kuwaongezea wasimamizi hao wa vivuko uelewa kuhusu taarifa na utabiri wa hali ya hewa, pamoja na umuhimu wa kuzingatia tahadhari za hali ya hewa katika uendeshaji wa vivuko ili kuimarisha usalama wa abiria na mali zao wakati wa kutoa huduma za usafiri majini wakati ambapo mvua kali zimetabiriwa kunyesha na huenda zikasababisha athari katika utoaji wa huduma ya vivuko.
Ushirikiano kati ya TEMESA, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ni muhimu katika kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinatumika ipasavyo katika kufanya maamuzi ya kiutendaji, kuzuia vihatarishi na kuimarisha utoaji wa huduma salama na endelevu za vivuko kote Nchini.