MUM KUTANGAMANISHWA NA NeST
Posted On: May 14, 2026
Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala, Bw. Moses Mabamba, akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TEMESA Bw. Kheri Mahimbali , amesema kuwa Mfumo wa Usimamizi wa Matengenezo (MUM) unatarajiwa kutangamanishwa na Mfumo wa Kielektroniki wa Manunuzi ya Umma (NeST) kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wadau wake pamoja na kuongeza ufanisi na uwazi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za matengenezo.
Mabamba ameyasema hayo tarehe 13 Mei, 2026 wakati wa kikao cha mashirikiano na maboresho ya mifumo baina ya TEMESA na PPRA kilichofanyika Mkoani Morogoro, amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuhakikisha huduma zinatolewa kwa haraka, uwazi na ufanisi.
“Utangamanishaji wa mifumo hii utaongeza ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa shughuli za matengenezo, kurahisisha usimamizi wa kazi pamoja na kuboresha michakato ya manunuzi inayohusiana na huduma mbalimbali zinazotolewa na TEMESA,” amesema Bw. Mabamba.
Aidha, ameongeza kuwa mfumo huo utawawezesha mafundi wabobezi kutoka katika Mikoa mbalimbali nchini kuomba kazi za umeme na matengenezo ambazo kwa sasa hazitekelezwi moja kwa moja na TEMESA, jambo litakalosaidia kuongeza ushindani, ubora wa huduma pamoja na kutoa fursa zaidi za ajira kwa wataalamu wa ndani.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mradi Mhandisi Pongeza Semakuwa, Meneja Kikosi cha Umeme TEMESA amesema kuwa kuunganishwa kwa mifumo hiyo kutarahisisha ufuatiliaji wa kazi, kupunguza urasimu usio wa lazima na kuongeza uwazi katika mchakato mzima wa utoaji wa huduma.
Mhandisi Pongeza, amewaomba wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono juhudi za mabadiliko zinazoendelea TEMESA ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali.