KIHENZILE ASISITIZA UMUHIMU WA KUIMARISHA USALAMA, UFANISI NA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA USAFIRI MAJINI
Posted On: September 26, 2026
Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile amefunga rasmi Maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani tarehe 24 Septemba, 2026 katika Viwanja vya Kijiji Ishirini na Moja, Jijini Tanga, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama, ufanisi na matumizi ya teknolojia katika sekta ya usafiri majini.
Akizungumza wakati kufunga maadhimisho hayo, Naibu Waziri amepongeza Mkoa wa Tanga, Wizara na wadau kwa kufanikisha maadhimisho hayo huku akisema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya sekta ya usafiri majini, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu, huduma za usafiri majini na kuongeza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma.
“Usafiri majini una nafasi muhimu katika kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii nchini, hususani katika maeneo yanayohudumiwa na usafiri huo hivyo ni muhimu kuzingatia matumizi sahihi ya teknolojia katika kuongeza ufanisi.” Amesema Mhe. Kihenzile.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta hiyo ambapo walipata fursa ya kuelimisha wananchi kuhusu huduma wanazotoa, usalama wa usafiri majini pamoja na fursa zilizopo katika sekta ya usafiri majini. TEMESA ni miongoni mwa taasisi zilizoshiriki katika maadhimisho hayo na kutoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala, ikiwemo huduma za vivuko, matengenezo ya magari, Ukodishaji wa mitambo, Ushauri wa Kihandisi pamoja na huduma za umeme na elektroniki.
Maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani, yaliyoanza tarehe 21 Septemba 2026 na kuhitimishwa tarehe 24 Septemba 2026 yamebeba kauli mbiu “Kutoka sera hadi utekelezaji: kuimarisha ubora katika Sekta ya Usafirishaji Majini”