KASEKENYA: WADAU WAKAE PAMOJA KUBORESHA MASLAHI YA MADEREVA
Posted On: September 19, 2026
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mha. Godfrey Kasekenya, amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kuzikutanisha Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara yenye dhamana ya Utumishi wa Umma, pamoja na taasisi zinazotoa mafunzo mbalimbali kwa madereva, ikiwemo Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), ili kujadili na kuona namna ya kuboresha maslahi ya madereva wa Serikali na kuondoa changamoto na manung’uniko yanayowakabili.
Mha. Kasekenya ametoa maelekezo hayo tarehe 16 Septemba 2026 wakati akifungua Kongamano la Tano la Madereva wa Serikali Tanzania, lililoambatana na maonesho yaliyofanyika katika viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Amesema madereva wana mchango mkubwa katika kuhakikisha shughuli za Serikali zinaendelea kwa ufanisi, hivyo kuna umuhimu wa wadau husika kukaa pamoja na kujadili changamoto zinazowakabili, ikiwemo masuala ya mafunzo, mazingira ya kazi na maslahi yao.
“Namuelekeza Katibu Mkuu Ujenzi kuzikutanisha Wizara zinazohusika pamoja na taasisi zinazotoa mafunzo kwa madereva kujadili kwa pamoja namna bora ya kuboresha maslahi yao na kuondoa manung’uniko,” amesema Mha. Kasekenya.
Katika kongamajo hilo, Mha. Kasekenya ametembelea pia banda la TEMESA na kupata fursa ya kujionea huduma na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Wakala, hususan katika matengenezo ya magari na vifaa vya kisasa ikiwemo Karakana inayotembea (Mobile Workshop).
Kongamano hilo limewakutanisha madereva wa Serikali kutoka maeneo mbalimbali nchini pamoja na wadau wa Sekta hiyo, likiwa na lengo la kujadili masuala ya taaluma ya Udereva, usalama barabarani, matumizi sahihi ya magari ya Serikali, teknolojia mpya za magari na namna ya kuongeza ufanisi katika utendaji wa Serikali.