WAZIRI KADOGOSA AIELEKEZA TEMESA KUIMARISHA MFUMO WA TIKETI ZA KIELEKTRONIKI KATIKA VIVUKO
Posted On: October 08, 2026
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa , amefanya ziara mkoani Arusha na kukutana na taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, ikiwa ni sehemu ya kuhimiza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Bw. Kheri A. Mahimbali, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Wakala.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mhe. Kadogosa ameielekeza TEMESA kuendelea na juhudi za kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato katika vivuko, hususan kushughulikia na kuimarisha mpango wa matumizi ya tiketi za kielektroniki, kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha huduma kwa wananchi wanaotumia vivuko.
Waziri Kadogosa amesisitiza umuhimu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maboresho ya mifumo, matumizi ya teknolojia na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
TEMESA itaendelea kutekeleza maelekezo hayo kwa kuimarisha matumizi ya teknolojia katika huduma za vivuko, sambamba na juhudi za kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa shughuli za Wakala.