MAONESHO YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA YAFUNGULIWA, TEMESA YAWEKA KAMBI
Posted On: September 27, 2026
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umeweka kambi katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bomba Mbili, mjini Geita, kwa lengo la kuwafikia wananchi na wadau wa sekta hiyo kwa kuwaelimisha kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala.
Maonesho hayo yamezinduliwa rasmi Septemba 27, 2026, na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven L. Kiruswa, huku TEMESA ikionesha huduma mbalimbali ikiwemo matengenezo na ukarabati wa magari, ukodishaji wa mitambo, huduma za umeme na elektroniki, ushauri wa kihandisi pamoja na matumizi ya mifumo ya kisasa katika usimamizi wa matengenezo.
Ushiriki wa TEMESA katika maonesho hayo unalenga kuimarisha uelewa kwa wananchi, taasisi, wachimbaji, wawekezaji na wadau wengine kuhusu umuhimu wa huduma za kihandisi katika kuongeza ufanisi wa shughuli za uzalishaji, hususan katika sekta ya madini.
Maonesho hayo yaliyobeba kaulimbiu: “Madini ni utajiri tuwajibike kwa pamoja kufika Dira ya taifa 2050" yanafanyika kuanzia Septemba 23 hadi Oktoba 3, 2026, yakishirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, wakiwemo wachimbaji, wawekezaji, wajasiriamali, taasisi za Serikali, taasisi za fedha pamoja na wazalishaji na wauzaji wa teknolojia na vifaa vya uchimbaji.