WAKAZI BUGOROLA - UKARA KIVUKO TAYARI MAJINI

News Image

Posted On: October 12, 2020

Wakazi wa Bugorola na Ukara wanatarajia kupelekewa kivuko kipya baada ya siku chache zijazo kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa kivuko cha MV. UKARA II HAPA KAZI TU. Kivuko hicho ambacho ujenzi wake umefanywa na kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine Transport ya jijini Mwanza kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 kimeshushwa majini leo kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kufanyiwa majaribio na vipimo kuangalia usalama wake kabla ya kupelekwa visiwani Ukerewe kwa ajili ya kuanza kutoa huduma.

Tukio la uteremshaji kwenye maji kivuko hicho limefanyika katika yadi ya Songoro iliyopo Ilemela mkoani Mwanza na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle, wakuu wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Mwanza, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wizara ya Ujenzi Mhandisi Lazaro Vazuri Pamoja na viongozi mbali mbali wa Wakala huo na wananchi wa maeneo hayo.

Akizungumza na waandishi wa Habari baada ya kuteremshwa kwa kivuko hicho Katibu Mkuu sekta ya Ujenzi Arch. Mwakalinga alisema anaishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuweza kutoa fedha ambazo zimetumika kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa kivuko hicho ambapo aliongeza kuwa mkoa wa Mwanza ni mkoa wa kimkakati na kwakuwa una visiwa vingi serikali haina budi kuwapelekea vivuko wakazi wa visiwa hivyo ili waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.

‘’Jumla serikali imetoa shilingi bilioni 15.3 kwa ajili ya ujenzi wa vivuko vyote vinne vipya, lakini kwa hapa Mwanza jumla yake imefikia bilioni 10’’. Aliongeza kuwa wataalamu kutoka nchi za nje waliomba kupewa tenda ya ujenzi wa kivuko hicho kwa gharama ya shilingi bilioni 22 na hivyo kuipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuamua wataalamu kutoka ndani ya nchi Songoro Marine watumike kujenga kivuko hicho na hivyo kuokoa Zaidi ya shilingi bilioni 18 ambazo zingezidi.

‘’Katika hili, nichukue fursa hii kuishukuru na kuipongeza sana kampuni ya Songoro Marine kwasababu wao ndio waliosema hapana, ni wazalendo wa hali ya juu, kutoka bilioni 22 kuja kufanya kwa bilioni 4.2 ni vizuri tuwapongeze’’. Alimaliza Katibu Mkuu.

Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle akizungumza na waandishi wa habari, alisema ujenzi wa vivuko vyote hivyo ilikuwa ni ahadi ya serikali ya Awamu ya Tano iliyoitoa kwa wananchi ambapo ilipanga kujenga vivuko vinne ikiwemo kivuko cha MV. Ilemela ambacho tayari kinatoa huduma, kivuko cha Mafia Nyamisati pamoja na kivuko cha Chato Nkome.

‘’Kivuko hiki kwa sifa yake kina urefu wa mita 42 na upana mita 10, kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 300 na magari 10 na hivi sasa kazi iliyobakia ni kupima uwezo wa kivuko hiki’’. Alisema Mtendaji Mkuu ambapo aliishukuru serikali kwa kutoa fedha zote zilizowezesha kukamilika kwa mradi huo ambapo aliongeza kuwa kukamilika kwa kivuko hiko ni ukombozi mkubwa sana kwa wakazi wa Bugorola Ukara ambao walikuwa wanasubiri kwa hamu ujio wa kivuko kipya.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella akizungumza katika tukio hilo alisema leo ni siku ya kihistoria akikumbushia kuzama kwa kivuko cha MV.Nyerereambapo Mhe. Rais Magufuli alitoa agizo kwa wizara husika la kujengwa kwa kivuko kipya baada ya kutokea kwa ajali hiyo, ‘’leo ni mashahidi, ndani ya takribani miaka miwili tu kamili kivuko hiki kimekamilika na sisi wote ni mashahidi, nchi yetu lazima tumshukuru Mungu sana kwa kupata kiongozi mahiri Dokta John Pombe Magufuli, ni mtu mwenye maamuzi, ni mtu mwenye maono na anayeguswa sana na shida za wananchi’’. Alisema Mhe. Mongela. Aliongeza kuwa fedha zote hizo zilizotumika kwa ujenzi wa vivuko hivyo ni fedha za ndani na wala sio fedha za msaada.

Kivuko cha MV.UKARA II kinatarajiwa kuanza kutoa huduma mara tu baada ya kukamilika kwa taratibu zote za ukaguzi na usalama ambazo zinafanywa na wataalamu mbalimbali ikiwemo wataalamu kutoka TASAC Pamoja na DMI.