MTENDAJI MKUU AWAAGIZA WATUMISHI TEMESA KUBUNI NAMNA BORA YA KUMRIDHISHA MTEJA

News Image

Posted On: April 23, 2022

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala amewaagiza watumishi wa Wakala huo kuhakikisha wanawajibika katika kupata mrejesho wa huduma wanazotoa kutoka kwa wateja wanaowahudumia ili kutafuta namna bora ya kuwaridhisha wateja hao. Mtendaji Mkuu amebainisha hayo wakati wa ziara yake ya kiutendaji aliyoifanya katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kutembelea karakana za Mikoa ya Iringa, Njombe, Songea, Mbeya ambapo pia alitembelea Wilaya ya kyela kukagua eneo la Kivuko ambapo Wakala unatarajia kupeleka kivuko kwa ajili ya kutoa huduma kati ya Mwaya na Kajunjumbele, Sumbawanga Rukwa, Katavi na Songwe kabla ya kumalizia ziara yake Mkoani Kigoma ambapo pia alipata fursa ya kutembelea kivuko cha MV. MALAGARASI kinachotoa huduma kati ya Ilagala na Kajeje Wilaya ya Uvinza.

Akizungumza na watumishi wa karakana za Mikoa hiyo kwa nyakati tofauti, Mtendaji Mkuu ambaye aliambatana na Mkurugenzi wa Matengenezo Mhandisi Hassan Karonda, amesema ni jukumu la kila mtoa huduma katika ofisi zote za Wakala kuhakikisha kwamba wateja wake wanaridhika kutokana na huduma wanazowapatia kwani ikitokea mteja hajaridhika kutokana na huduma aliyopatiwa basi kuna uwezekano mkubwa kumpoteza mteja huyo.

‘’Mtoa huduma yeyote siku zote huwaga anaangalia wale wadau wake wanaridhika kwa kiasi gani na zile huduma zake, na pale anapoona wadau wake wana kutokuridhika katika eneo fulani basi inakua ni jukumu lake mtoa huduma kuona ni namna gani anabadilika ili kuongeza kuridhika kwa wateja kwasababu wateja wasiporidhia huduma haiwezi kuwa na uendelevu’’, alisema Mtendaji Mkuu ambapo aliongeza kuwa TEMESA ina wadau wakubwa watatu ambao ni Serikali kwa maana ya wamiliki wa TEMESA, taasisi za Serikali ambazo TEMESA unawatengenezea magari pamoja na Wazabuni ambao wanaiwezesha TEMESA kufanya kazi zake kwa kuipatia vifaa vya kufunga kwenye magari ya wateja wake.

Aidha, akiwa katika ziara hiyo, Mtendaji Mkuu amebainisha kwamba kuna changamoto kubwa katika suala la upatikanaji wa vifaa ambalo linachagizwa na mahusiano kati ya Wakala na Wazabuni, lakini pia changamoto nyingine ni kuhusu namna gani wanaotengenezewa magari na TEMESA wanaridhishwa na zile huduma ambazo wanapatiwa kwenye karakana za Wakala huo, Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa kwa kiasi kikubwa wateja wamekuwa na manung’uniko makubwa kuhusu kazi wanazofanyiwa.

‘’Ni wajibu wetu kama watoa huduma, tufungue masikio, tuwasikie, tupate ule mrejesho kutoka kwao, pale ambapo tunaona maeneo hayo wateja wetu hawaridhiki basi tutafute mikakati bora ya kurekebisha ili mwisho wa siku wateja wetu waridhike, wateja wetu wakiridhika wataweza kutulipa kwa wakati, wakiweza kutulipa kwa wakati nasisi tutaweza kuwalipa wazabuni wetu kwa wakati lakini hayo yote yakienda vizuri maana yake na Serikali nayo itakuwa inaridhika kwamba Taasisi niliyoianzisha kwa matarajio Fulani basi inayishi yale matarajio’’. Alimaliza Mtendaji Mkuu na kusisitiza kwamba Wakala una kazi kubwa ya kufanya kwakuwa maeneo hayo bado hayajakaa vizuri.

Aidha Mtendaji Mkuu aliwaagiza watumishi hao pamoja na mameneja wao kuhakikisha kwamba yale maeneo yote ambayo wanalalamikiwa kwa kiasi kikubwa wahakikishe wanatengeneza mikakati ya kuyarekebisha huku akisisitiza kwamba kwa upande wao kama Makao Makuu watajitahidi kupunguza malalamiko kwa kuchukua hatua kadha wa kadha ambapo hatua moja kubwa ambayo imeichukua ni kuanza utaratibu mpya wa ununuaji wa vipuri kwa kuanza sasa kununua vipuri hivyo kutoka kwa wazabuni wakubwa ambao watauhakikishia Wakala unapata vipuri kwa bei ya kueleweka lakini kwa uhakika zaidi na kwa wakati.

Nao Mameneja wa Mikoa husika pamoja na watumishi wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara hiyo, wamebainisha changamoto mbalimbali ambazo wanakutana nazo katika utendaji kazi wao wa kila siku ambapo miongoni mwa changamoto walizozibainisha ni pamoja na upungufu wa watumishi katika kada mbalimbali ikiwemo mafundi, uchakavu wa karakana pamoja na ofisi, ukosefu wa magari kwa ajili ya kufanyia mizunguko mbalimbali, ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kununulia vipuri ambavyo vitachochea kasi ya kiutendaji pamoja na suala la madeni ambalo limeonekana kuzidi kuwa kubwa kwa upande wa karakana husika.

Mtendaji Mkuu akijibu baadhi ya hoja hizo, aliwaagiza mameneja wa mikoa hiyo kuhakikisha wanajitafakari hasa katika upande wa ukusanyaji wa madeni pamoja na uzalishaji kwani wakifanikiwa katika hayo wataweza kuajiri watumishi wa mikataba maalumu katika kada ambazo zina upungufu lakini pia wataweza kulipa madeni ya wazabuni ambayo wanadaiwa. ‘’Chochote tunachotamani kukifanya kitawezekana kama tu tumefanya vizuri katika ukusanyaji na uzalishaji, tunapoongelea makusanyo ya Mkoa hapa kila mmoja ajue hii ni ajenda inayomuhusu yeye kama yeye, hakuna mtu wa kutuletea hela hapa, sisi ndio tunazalisha hizo hela’’, Alimaliza Mtendaji Mkuu.

Tanzania Census 2022