BILIONI 2.9 ZAKARABATI VIVUKO VYA MV. SENGEREMA NA MV. TEGEMEO

News Image

Posted On: August 19, 2021

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) imekamilisha mradi wa ukarabati wa vivuko viwili vinavyotoa huduma Mkoani Mwanza kwa gharama ya shilingi Bilioni 2.9.

Vivuko hivyo, MV. SENGEREMA kinachotoa huduma kati ya Kigongo Wilayani Misungwi na Busisi Wilayani Sengerema na MV. TEGEMEO kinachotoa huduma kati ya Kaunda Maisome na Kanoni Halmashauri ya Buchosa Wilayani Sengerema, vimefanyiwa ukarabati mkubwa baada ya kufikia muda wake wa kufanyiwa ukarabati ambayo imekuwa ni desturi inayofanywa na Wakala huo mara kwa mara ili kuhakikisha vivuko hivyo vinaendelea kutoa huduma bora wakati wote vikiwa katika hali ya usalama.

Akizunguma na waandishi wa habari mapema leo katika hafla fupi za kupokea vivuko hivyo zilizofanyika katika kivuko cha Kigongo Busisi mjini Mwanza ambapo kilipokelewa kivuko cha MV. SENGEREMA na Pasiansi Ilemela katika yadi ya Songoro kilipopokelewa kivuko cha MV.TEGEMEO, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, amesema kivuko cha MV. SENGEREMA kilibainika kuwa na uchakavu mkubwa zaidi na hivyo kupelekewa kutolewa kwenye maji kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa mapema iwezekanavyo.

‘‘Kivuko kilipotolewa kwenye maji ili kazi ya ukarabatiianze kilibainika kuwa na uchavu mkubwa zaidi, hivyo kupelekea kuandaa mapitio mapya (addendum) yaliyopelekeakivuko kufungwa injini mbili mpya pamoja na propulsion unit mbili mpya zilizogharimu USD 790,550.15 sawa na TZS 1,809,956,662.92. Mabadiliko ya mkataba huu yalifanya kazi ya ukarabati kuanza rasmi tarehe 22 Aprili, 2020 kwa gharama ya TZS 2,249,181,662.92‘‘. Alisema Mhandisi Maselle na kuongeza kuwa kivuko hicho kimefungwa injini mbili mpya aina ya Marine Doosan Engine Infracore zikiwa na gearbox zake ambazo uwezo wake ni Horse Power (HP) 285 kila moja.

‘’Vile vile kivuko hiki kimewekewa vifaa vya kisasa vya kukiongoza kama Radar, GPS, Magnetic Compass, vifaa vya mawasiliano (Communication Equipment) na vifaa vya uokoaji vya kutosha kwa watu wazima na watoto ambavyo ni makoti ya kujiokoa (life jackets) na maboya (life buoys)’’. Alimalizia Mtendaji Mkuu.

Aidha, mara baada ya kupokea kivuko cha MV. SENGEREMA, tukio lililofuata lilikua ni kupokea kivuko kingine cha MV. TEGEMEO, shughuli iliyofanyika katika yadi ya Songoro iliyopo Pasiansi Ilemela Mkoani Mwanza ambapo huko pia Mhandisi Maselle alipata wasaa wa kuzungumza na waandishi wa habari ambapo aliwapa taaarifa fupi kuhusu ukarabati wa kivuko hicho.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, Mhandisi Maselle amesema kampuni ya kizalendo ya M/S SONGORO MARINE TRANSPORT LTD ya jijini Mwanza ilishinda zabuni ya ukarabati wa kivuko hicho kwa gharama ya Shilingi milioni 672,417,900.00 za Kitanzania ambapo ilianza kazi hiyo mara moja ili kuhakikisha wananchi wanaotegemea kivuko hicho wanakipata baada ya muda mfupi zaidi.

‘’Kivuko hiki kimefungwa injini mbili mpya aina ya Marine Doosan Engine Infracore zikiwa na gearbox zake ambazo uwezo wake ni Horse Power (HP) 300 kila moja kina uwezo wa kusail siyo chini ya 9kn. Vile vile kivuko hiki kimewekewa vifaa vya kisasa vya kukiongoza kama Radar, GPS, Magnetic Compass, vifaa vya mawasiliano (Communication equipment) na vifaa vya uokoaji vya kutosha kwa watu wazima na watoto ambavyo ni makoti ya kujiokoa (life jackets) na maboya (life buoys)’’. Alisema Mtendaji Mkuu ambapo aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya huduma za vivuko na kuahidi kuendelea kutunza vivuko hivyo kwa kuvifanyia matengenezo kama inavyotakiwa ili viweze kudumu na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Songoro, Major Songoro akizungumza katika hafla hiyo fupi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuiamini na kuipa zabuni za kutengeneza na kukarabati vivuko na kuahidi kuendelea kufanya kazi yenye viwango na ubora uliotukuka.

Kivuko cha MV. SENGEREMA kina uwezo wa kubeba abiria 490 na magari 24 sawa na tani 170, kina urefu wa mita 55, upana wa mita 10.5 na kina cha kuelea mita 1.4, wakati Kivuko MV. TEGEMEO kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 85, urefu wa mita 37, upana wa mita 10 na kina cha kuelea mita 0.75.

Fedha zote zilizotumika kukarabati vivuko hivyo zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.