TEMESA YAFANYA UKAGUZI MAGARI YA SERIKALI KUJIANDAA NA MKUTANO MKUU WA MABUNGE DUNIANI
Posted On: September 23, 2026
Kikosi cha Wahandisi kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na kikosi cha Wahandisi kutoka TEMESA Makao Makuu Dodoma, tarehe 22 Septemba, 2026 kimefanya zoezi maalum la ukaguzi wa magari ya Serikali yanayotarajiwa kutumika katika Mkutano Mkuu wa Mabunge ya Dunia (IPU). Ukaguzi huo unaolenga kuhakikisha usalama wa vyombo vya moto, umefanyika katika Viwanja vya Soweto - Mianzini, Jijini Arusha, Jiji linalotarajiwa kuwa mwenyeji wa wageni mbalimbali kutoka nchi zaidi ya 100 duniani
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Msimamizi wa zoezi Mhandisi Jafari Kalasi wa TEMESA Arusha amesema ukaguzi huo ni sehemu ya maandalizi ya mapema kuhakikisha magari yote yatakayotumika kwenye mkutano huo mkubwa wa kimataifa unaotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Oktoba, yanakuwa katika hali ya usalama na ubora wa hali ya juu.
"Tumeshirikiana kama timu moja Arusha na Dodoma kuhakikisha tunakagua kila gari kwa umakini, lengo letu ni kuhakikisha wageni wetu watapata huduma bora na salama ya usafiri kwa kuwa na usafiri salama" amesema Mhandisi Karasi
Zoezi la ukaguzi linaendelea kwa siku kadhaa ili kuhakikisha hakuna gari lenye hitilafu litakaloingia barabarani wakati wa mkutano huo. Miongoni mwa magari yaliyokaguliwa ni pamoja na magari ya kubebea wageni, magari ya ulinzi na magari ya dharura. TEMESA imehaidi kuendelea kutoa “HUDUMA BORA ZINAZOLETA FURSA ZA MAENDELEO" kama kauli mbiu yake inavyosema.