Naibu Waziri Ujenzi aitaka TEMESA kutumia mifumo ya Kielektroniki kivukoni
Posted On: April 16, 2019
NAIBU Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), kufanya kazi kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kieletroniki ili kuimarisha usalama na kuongeza ukusanyaji wa mapato katika huduma zake.
Naibu Waziri Kwandikwa amesema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa TEMESA, na kusisitiza umuhimu wa kila mfanyakazi kufikiria usalama na uboreshaji wa huduma katika eneo lake la kazi.
"Hakikisheni mifumo yote ya kimawasiliano na kimapato inaunganishwa pamoja ili iwe rahisi kufuatilia ubora na uhakika wa huduma zenu nchini kote na hivyo kuwawezesha kutoa huduma bora," amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.
Amewataka TEMESA kuhakikisha inaongeza imani kwa wateja wake kwa kutoa huduma bora wakati wote na kudhibiti rushwa na uzembe katika utendaji wa kazi wa siku kwa siku.
Aidha, Naibu Waziri huyo amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TEMESA kuhakikisha watumishi wote wa wakala huo wanapata fursa za mafunzo ili kuwiana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoendelea duniani na hivyo kutoa huduma yenye tija kwa wakati.
Naye Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Masele amesema taasisi yake imejipanga kukusanya madeni ya huduma ilizozitoa kwa wakati na kupeleka huduma hizo pia katika maeneo ya wilaya ili kuongeza wigo wa huduma zake kwa wananchi. Amesisitiza kuwa TEMESA itaendelea kujenga vivuko vipya na kukarabati baadhi ya karakana zake ili kutoa huduma bora na za haraka kwa wananchi.
Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la TEMESA uliofunguliwa siku ya Tarehe 12 Aprili mwaka huu, pamoja na mambo mengine umepitisha dira, mwelekeo na makadirio ya bajeti ya wakala huo kwa mwaka wa fedha 2019/20.