TEMESA YARIDHISHWA MAENDELEO YA UJENZI WA KIVUKO KIPYA CHA MAFIA–NYAMISATI
Posted On: September 11, 2026
Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ujenzi wa Vivuko kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mhandisi Lukombe King’ombe, leo tarehe 11 Septemba, 2026 amefanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa kivuko kipya kinachojengwa kwa ajili ya kutoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati Mkoani Pwani, huku ukieleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mhandisi King’ombe amesema lengo la ziara hiyo ni kukagua maendeleo ya ujenzi wa kivuko hicho ambacho kinatarajiwa kuwa kivuko cha pili katika eneo la Mafia na Nyamisati, ikiwepo MV. KILINDONI na kuongeza wigo na uwezo wa usafiri kwa wananchi wa Mafia na Nyamisati. Mhandisi King’ombe amesema ukaguzi umebaini kuwa kazi inaendelea vizuri, ambapo baadhi ya mitambo kama jenereta, zimeanza kufungwa na kufanyiwa msawazo huku kazi nyingine zikiendelea katika maeneo mbalimbali ya kivuko.
“Leo tumeangalia maendeleo ya kazi na tumedhihirisha kwamba maendeleo ni mazuri, tumeona jenereta zimeanza kufungwa katika maeneo yake na zinafanyiwa msawazo (allignment) ili kukamilisha kazi, pia tumeona ufungaji wa vifaa vya uongozaji wa meli, waya za umeme pamoja na mabomba ya maji,” amesema Mhandisi King’ombe. Ameongeza kuwa timu hiyo imekagua eneo la nahodha (control room), ambapo vifaa vya udhibiti tayari vimewekwa na kazi ya kuunganisha nyaya inaendelea ili mitambo yote itakapowashwa kivuko kiwe tayari kwa majaribio ya awali.
Kwa mujibu wa Mhandisi King’ombe, ujenzi wa kivuko hicho umefikia hatua nzuri, hivyo amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi kwa kufanya kazi usiku na mchana, ili kukamilisha kazi zilizobaki na kivuko hicho kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi wa Mafia, ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za usafiri katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Mhandisi Lazaro Isack, Mhandisi wa Mitambo ya Meli kutoka Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ambao ni washauri elekezi, watahakikisha ujenzi wa kivuko unafanyika kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa pamoja na kuonesha thamani ya fedha (value for money). Amesema kivuko hicho kinajengwa kwa mfumo wa blocks, ambapo kwa sasa blocks zote zimefikia hatua kubwa ya kukamilika.
“Kwa upande wetu kama mshauri elekezi, kazi yetu ni kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa kiwango kinachotakiwa, lakini pia kuhakikisha kunakuwa na thamani ya fedha inayotolewa na Serikali katika ujenzi wa kivuko hiki,” amesema Mhandisi Lazaro.
Naye Mhandisi Benjamin Msabaha, Mhandisi wa Meli kutoka kampuni ya Dar es Salam Merchant Group (DMG), amesema ujenzi wa kivuko hicho umefikia asilimia 74. Amesema vifaa muhimu kwa ajili ya kukamilisha kivuko hicho vimefika, vikiwemo injini, jenereta, pampu za maji, mifumo ya maji safi, mifumo ya mafuta pamoja na mifumo ya upoozaji. Ameongeza kuwa vifaa vingine vilivyofika ni pamoja na ngazi, waya, matrei ya waya na mifuniko ya waya, huku vifaa vya vyumba vya manahodha, ikiwemo paneli za silingi na kuta za panelo, vikiwa vinaendelea kuagizwa.
“Kwa ujumla, tunatarajia vifaa vilivyobaki kufika ifikapo mwisho wa mwezi wa kumi, ili kukamilisha mradi ndani ya muda uliopangwa,” amesema Mhandisi Msabaha. Amesisitiza kuwa wao kama wakandarasi wataendele kuongeza kasi ya ujenzi huku wakizingatia ubora, ili kivuko hicho kikamilike na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Mafia na Nyamisati.
Kivuko kipya cha Mafia Nyamisati kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 300 na magari madogo kumi sawa na tani 120.