​TEMESA YAWEKA TEKNOLOJIA ZA MAGARI MBELE KATIKA KONGAMANO LA TANO LA MADEREVA

News Image

Posted On: September 19, 2026

MADEREVA wa Serikali wamepata elimu kuhusu teknolojia mpya za magari na mifumo ya kisasa ya usimamizi wa magari, hatua inayolenga kuongeza ufanisi, usalama na kupunguza gharama za uendeshaji wa magari ya Serikali. Elimu hiyo imetolewa na Mhandisi Charles Mbogolo kutoka TEMESA katika Kongamano la Tano la Madereva wa Serikali Tanzania, linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mhandisi Mbogolo ameeleza kuwa teknolojia ya magari ya hybrid, ambayo inachanganya matumizi ya injini ya mafuta na mfumo wa umeme, inawezesha kupunguza matumizi ya mafuta na gharama za uendeshaji, huku ikisaidia kuongeza ufanisi na matumizi bora ya magari.

“Uelewa wa teknolojia mpya za magari ni muhimu kwa madereva na watumiaji wa magari ili waweze kutumia teknolojia hizo kwa usahihi, kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji,” amesema Mhandisi Mbogolo.

Aidha, Mhandisi Mbogolo ametoa elimu kuhusu mifumo ya MUM na NEST, akieleza namna mifumo hiyo inavyosaidia kuboresha usimamizi, ufuatiliaji na ufanisi wa matumizi ya magari ya Serikali.

Madereva wameelekezwa kuzingatia taratibu za matumizi ya magari ya Serikali, kutoa taarifa mapema pale wanapobaini hitilafu na kuhakikisha magari yanafanyiwa matengenezo kwa kuzingatia ratiba na mahitaji ya kitaalamu.

Sambamba na kongamano hilo, TEMESA imeshiriki katika maonesho yanayoambatana na Kongamano la Tano la Madereva wa Serikali Tanzania, yanayofanyika katika eneo la Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Kupitia maonesho hayo, TEMESA inatoa fursa kwa madereva, washiriki na wadau mbalimbali kupata taarifa kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala, ikiwemo matengenezo ya magari na mitambo, mifumo ya usimamizi wa matengenezo pamoja na huduma mbalimbali za kihandisi.

Ushiriki wa TEMESA katika kongamano na maonesho hayo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa magari ya Serikali, kutangaza huduma za Wakala na kuimarisha ushirikiano na wadau katika kuboresha usimamizi, matumizi na matengenezo ya magari ya Serikali.