TEMESA YAIMARISHA UWEZO WA MAFUNDI NA WAHANDISI KUKABILI MABORESHO YA MFUMO
Posted On: September 15, 2026
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umeanza kikao kazi cha siku mbili cha kuwajengea uwezo mafundi na wahandisi kuhusu maboresho yanayofanyika katika mfumo wa taasisi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ufanisi na ubora wa utoaji wa huduma.
Kikao hicho kimefanyika Septemba 14, 2026, katika Ofisi za Makao Makuu ya TEMESA jijini Dodoma na kimehudhuriwa na mafundi pamoja na wahandisi kutoka katika ofisi mbalimbali za Wakala Mikoani.
Akifungua kikao hicho, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Bi. Safinael Mapesa, amewataka washiriki kutumia kikamilifu fursa hiyo kwa kushirikishana uzoefu, kusikiliza na kuelewa maboresho yanayofanyika katika mfumo huo.
Amesisitiza umuhimu wa washiriki kuelewa vyema mafunzo hayo ili watakaporejea katika vituo vyao vya kazi waweze kuwafundisha na kuwajengea uwezo wenzao, hivyo kuhakikisha maboresho hayo yanaeleweka na kutumika kwa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
“Ni muhimu kushirikishana uzoefu, kusikiliza na kuelewa vizuri maboresho haya ili mtakaporejea katika vituo vyenu vya kazi muweze kuwafundisha wenzenu,” amesema Bi. Mapesa.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Meneja wa Umeme na Elektoniki TEMESA, Mhandisi Pongeza Semakuwa, ambaye anawaelekeza washiriki kuhusu maboresho mbalimbali ya mfumo pamoja na namna bora ya kuyatumia katika kurahisisha na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.