KATIBU MKUU WIZARA YA UJENZI ATEMBELEA TEMESA, TAADHARI EL NIÑO YATOLEWA
Posted On: September 15, 2026
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mh.Balozi Dkt. Aisha Amour, ametembelea ofisi za Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) mkoani Pwani na kuwataka kujiandaa mapema kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa na athari za hali ya hewa ya El Niño.
Akizungumza wakati wa ziara yake Mkoani Pwani, Mh. Balozi Dkt. Aisha Amour amesema maandalizi ya mapema ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa watumishi, mali za Serikali na mwendelezo wa huduma wakati wa mvua kubwa.
Amesema TEMESA inapaswa kuhakikisha magari yaliyoharibika au yaliyoachwa katika maeneo ya barabarani yanaondolewa na kurejeshwa katika taasisi husika, huku zana na vifaa vilivyokaa kwa muda mrefu vikirejeshwa na kuwekwa katika hali ya matumizi.
“Tusisubiri mvua kubwa zianze ndipo tuchukue hatua. Tunapaswa kujiandaa mapema na kuhakikisha maeneo yetu yako salama,” amesema Mhe. Balozi Dkt. Amour.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya TEMESA, TANROADS na TBA, hususan katika kutumia kwa pamoja wataalamu, zana na rasilimali zilizopo ili kukabiliana kwa ufanisi na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Amesema maandalizi hayo yatawezesha taasisi hizo kuimarisha usalama wa miundombinu na mali za Serikali, kulinda watumishi pamoja na kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi katika kipindi cha mvua kubwa.