TAARIFA KWA UMMA

Imewekwa Friday 17th Feb , 2023

TAARIFA KWA UMMA

Siku ya tarehe 16/02/2023 Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ulisaini mkataba wa Ukarabati Mkubwa wa kivuko Mv Magogoni na Mkandarasi African Marine General Enterpises ya Mombasa, Kenya wenye gharama ya TZS 7,572,302,496.00 (pamoja na VAT). Mkandarasi huyu alipatikana baada ya kufanyika ushindani wa kimataifa (International Tendering) na kushinda kwa kigezo cha bei (lowest evaluated bidder) akiwa ameweka gharama ya TZS 7,572,302,496.00 wakati Mkandarasi aliyefuatia aliweka gharama ya TZS 10,958,187,440. Aidha, tathmini ya tender pia ilizingatia uwezo na uzoefu wa kufanya kazi ambapo mkandarasi huyu alithibitika kukidhi vigezo hivyo pia.

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) unapenda kutoa ufafanuzi wa gharama za ukarabati wa kivuko MV Magogoni ili kuongeza uelewa kwa wananchi ambao wanafuatilia jambo hili kwa umakini mkubwa:

  • Kivuko MV Magogoni kilijengwa mwaka 2008 na Kampuni ya Neuer Ruhrorter Schiffswert ya Ujerumani kwa gharama ya Euro 5,287,800. Wakati huo Euro moja ikibadilishwa kwa Shilingi za Tanzania 1,756.78 hivyo gharama hiyo ilikuwa sawa na TZS 9,289,501,284 (yaani Euro 5,287,800 x 1,756.78). Ukarabati mkubwa wa Mv Magogoni unafanyika mwaka 2023 kwa gharama ya TZS 7,572,302,496.00 wakati huu Euro moja inabadilishwa kwa Shilingi za Tanzania 2,487.786 hivyo gharama hii ni sawa na Euro 3,043,791.7 au 57.56% ya gharama ya ununuzi wa kivuko. Gharama hii ya Ukarabati pia inajumuisha vipuri vya ziada vya injini, kusafirisha kivuko kwenda Mombasa na kurudi Dar es Salaam baada ya ukarabati pamoja na ukaguzi wa kivuko kikiwa Mombasa.

Inatupasa kufanya ulinganifu wa gharama hizi kwa fedha za kigeni kwa kuwa vifaa vyote vinavyofanikisha ukarabati mkubwa wa kivuko vinanunuliwa toka nje ya nchi kama inavyoainishwa hapa chini

NA

KIFAA

Nchi kinakonunuliwa

1.

Marine SteelPlates

Dubai

2.

Catapillar Engine

UK

3.

Gear Box

UK

4.

PropulsionSystem - Schotel

Germany

5.

Lifesaving Appliances

India

6.

Vifaa vya umeme na kielektroniki

India

  • Ukiachilia mbali mabadiliko ya viwango vya kubadili fedha baina ya Shilingi ya Tanzania na fedha za kigeni (Euro) sababu nyingine ya gharama hii kubwa ni kupanda kwa bei ya soko ya vifaa hivi baina ya mwaka 2008 na mwaka 2023. Tathmini iliyofanywa kwa kuzingatia bei za soko za mwaka 2022 inaonesha kuwa kujenga kivuko kipya sawa na MV Magogoni (Tani 500, Abiria 2,000) kwa sasa (mwaka 2023) kitagharimu kiasi kisichopungua Shilingi za Tanzania Bilioni 25.
  • Aidha, kwa kuwa ukarabati mkubwa wa kivuko unajumuisha ununuzi wa vifaa vipya (kama ilivyokuwa wakati wa Ujenzi/ununuzi wa kivuko) gharama za ukarabati zinakuwa kubwa tofauti na matengenezo ya kawaida.

Imetolewa na Kitengo cha Masoko na Uhusiano

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA)

17.02.2023